Mkoa wa Mtwara mwenyeji Kitaifa, Wiki ya Uhamasishaji wa Elimu Tanzania (24- 28 Aprili 2017)

Kwa muda Mrefu Mikoa ya Kusini mwa Tanzania, Mtwara na Lindi inatajwa kuwa na kiwango cha chini Kielimu kutokana na sababu mbalimbali, ambapo matokeo ya mwaka 2016 yamekuwa mabovu zaidi kuanzia ngazi ya msingi mpaka Sekondari (shule zaidi ya tano kati ya kumi zilizofanya vibaya Form Two zilitokea Mtwara).
Inawezekana hii ni moja kati ya sababu zilizowavuta waratibu na waandaji wa Global Action Week for Education (GAWE) 2017- Wiki ya Maadhimisho yaUhamasishajiwa Elimu (WIKI YA ELIMU) 2017, kuamua kuuchagua mkoa wa Mtwara kuwa mwenyeji wa wiki hii kwa mwaka huu 2017.
Wiki hii itatumika kuikumbusha serikali, jamii na mashirika yasiyo ya Kiserikali yanayojishughulisha na elimu, wajibu wao katika kutekeleza Malengo ya Maendeleo endelevu hasa lengo la 4 na 5, Pia itakumbusha kuwa na mipango madhubuti ya utekelezaji wa lengo la nne na tano.
Lengo ni kuondoa changamoto kama vile; Mila na desturi zinazorudisha nyuma utoaji wa elimu bora , Jamii kukosa mwamko wa kushiriki katika masuala ya shule, Fedha ndogo zinazotolewa na Serikali kwa elimu n.k.
Kaulimbiu katika ngazi ya kitaifa ni “Uwajibikaji kwa Lengo la Maendeleo Endelevu lengo namba Nne (SDG4) na Ushiriki wa Wananchi (Accountability for SDG4, and Active Citizen Participation)” ambapo matokeo chanya yanayotarajiwa ni Kuona uwajibikaji wa pamoja, Kuongezeka mwamko wa elimu , Kupunguza utoro, Mipango ya kuongeza idadi ya walimu mkoani wa Mtwara na Kuongezeka ufaulu wa wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari Nanyumbu na Mtwara kwa ujumla
Maadhimisho haya yalianza mara baada ya Mkutano Mkuu wa pili wa kiulimwengu ambao ulifanyika Dakar Senegal mwaka 2000 na Kila nchi hufanya maadhimisho hayo katika wiki iliyopangwa na waratibu ambao ni Global Campaign for Education” (GCE)
Kwa Tanzania wiki hii inaandaliwa kwa zaidi ya miaka kumi na moja sasa na TEN/MET kwa kushirikiana na wadau wengine wa elimu nchini na Mwenyekiti wa Kamati kwa mwaka huu ni Shirika la HakiElimu.

Leave a Reply